You are on page 1of 42

1

CHECK AGAINST DELIVERY


HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA
WANANCHI, TAREHE 31 JULAI, 2014
Utangulizi
Ndugu wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kwa
mara nyingine tena kuzungumza na taifa juu ya masuala
muhimu yanayohusu nchi yetu. Mwezi wa Saba tunaoumaliza
leo ulikuwa na matukio mengi baadhi yakiwa makubwa na
kushtusha na mengine yalikuwa matukio ya kawaida.
Mashambulio ya Mabomu
Ndugu Wananchi;
Tarehe 3 Julai, 2014 na tarehe 07 Julai, 2014 kulitokea
mashambulizi ya mabomu nyumbani kwa Sheikh Sudi Ally
Sudi na katika mgahawa wa Vama kwa mfuatano huo. Kabla
ya hapo, kulikuwa na matukio mengine matatu: Kanisa la
Olasiti tarehe 5 Mei, 2012, Mkutano wa Kampeni wa
2
CHADEMA tarehe 15 Juni, 2013 na Baa ya Arusha Night Park
tarehe 13 Aprili, 2014. Hali kadhalika, tarehe 13 Juni, 2014
kulitokea shambulizi la mabomu katika eneo la Darajani,
Zanzibar.
Kila lilipotokea shambulizi uchunguzi ulifanyika na
watuhumiwa kukamatwa. Lakini, watuhumiwa waliokamatwa
safari hii wanaelekea kutoa sura nzuri zaidi ya mtandao wa
watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili pale Arusha na
kwingineko nchini. Watu 38 wameishafkishwa Mahakamani,
wengine 8 watafkishwa Mahakamani kesho na uchunguzi na
msako unaendelea kote nchini kuwapata watuhumiwa
wengine.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri
iliyotufkisha hapa tulipo sasa. Tunawaomba waongeze bidii,
maarifa na ushirikiano mpaka wote waliohusika wakamatwe
na kufkishwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha, natoa pongezi na shukrani maalum kwa wananchi
wema waliotoa taarifa zilizowezesha kukamatwa kwa
3
watuhumiwa. Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wananchi
wenye taarifa kuhusu wanaotafutwa au ye yote anayejihusisha
na vitendo hivi viovu watoe taarifa kwenye vyombo vya
usalama ili hatua zipasazo zichukuliwe.
Kutupwa Viungo vya Binadamu
Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Julai, 2014, katika Bonde la Mto Mpiji lililopo
eneo la Bunju Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam,
viligunduliwa viungo vya binadamu na baadhi ya vitendea
kazi vya madaktari vikiwemo aprons na gloves. Viungo hivyo
vilivyokutwa vimekakamaa na kuhifadhiwa katika mifuko
myeusi 85, vilikuwa vimetupwa jana yake tarehe 21 Julai, 2014.
Tukio hilo lilileta taharuki na hofu kubwa katika Jiji la Dar es
Salaam na nchini kwa ujumla.
Uchunguzi uliofanywa uligundua kuwa viungo hivyo
vilikuwa vinatumika kufundishia wanafunzi wa udaktari
katika Chuo Kikuu cha Tiba kilichoko Mbezi Beach maarufu
kwa jina la IMTU. Ni utaratibu wa kawaida kwa vyuo vikuu
vya udaktari nchini na kote duniani kutumia miili ya
4
wanadamu waliofariki kufundishia. Hata hivyo, pale viungo
hivyo vinapokuwa havihitajiki tena kwa shughuli hiyo, zipo
taratibu zake za kuvisitiri ambazo hazikufuatwa. Bahati nzuri
mamlaka husika zimeona kasoro hiyo na hatua zimeanza
kuchukulikuwa. Tuziachie mamlaka hizo kuchukua hatua
zipasazo kwa mujibu wa madaraka yao na kwa mujibu wa
Sheria na Kanuni zinazotawala shughuli za namna hiyo. Ni
matumaini yangu kuwa yaliyofanywa na IMTU hayatafanywa
tena na Chuo hicho wala chuo kingine cho chote hapa nchini.
Ziara Yangu Mikoani
Ndugu Wananchi;
Katika mwezi huu wa Julai, nimefanya ziara katika ya
mikoa ya Tanga na Ruvuma. Nimefurahishwa sana na hatua
kubwa ya maendeleo waliyopiga wananchi wa mikoa hiyo.
Pamoja na mchango wa Serikali, ari na mwamko mkubwa wa
kujiletea maendeleo walionao viongozi na wananchi wa mikoa
hiyo vimechangia sana katika kuongeza kasi ya maendeleo na
mafanikio yanayoendelea kupatikana. Katika ziara hizo,
nilizindua miradi iliyokamilika na kuweka mawe ya msingi ya
5
ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya
barabara, umeme,maji, afya, elimu, majengo ya Serikali,
nyumba na kadhalika.
Nimepata faraja kubwa kupata taarifa kuwa ahadi zangu
nyingi na zile zilizomo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi
zimekamilika na zingine ziko katika hatua mbalimbali za
utekelezaji. Ndoto ya miaka mingi, kabla na baada ya Uhuru,
ya wananchi wa Mikoa ya Kusini ya kutaka Mikoa yao
ifunguke na kuunganishwa na mikoa mingine kwa barabara za
lami sasa kuna uhakika wa kukamilika. Barabara ya kutoka
Mbinga, Songea hadi Namtumbo iliyojengwa kwa msaada wa
Serikali ya Marekani imekamilika na tuliizindua. Tuliweka
mawe ya msingi ya kujenga barabara ya lami kutoka
Namtumbo, Tunduru, Mangaka hadi Mtambaswala kwenye
Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa
msaada wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali ya Japan.
Barabara ya kutoka Mangaka hadi Masasi iliyojengwa kwa
msaada wa Serikali ya Japan imekamilika na tuliizindua.
Katika barabara ya kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay kimebaki
6
kipande cha kilometa 66 kutoka Mbinga kwenda Mbamba Bay
ambacho hakikuwa na mpango wo wote wa kuwekewa lami
kwa sasa. Bahati nzuri, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (ADB), Bibi Tonia Kandiero alitangaza
pale Namtumbo kuwa Benki yake itafadhili ujenzi wa barabara
hiyo. Mambo sasa yamekamilika.
Kule Masasi mkoani Mtwara na Nachingwea mkoani
Lindi tulizindua kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa
Mbwinji unaomaliza tatizo kubwa la maji kwa miji hiyo kwa
miaka mingi ijayo.
Nyumba za Bei Nafuu
Ndugu Wananchi;
Nikiwa wilayani Mkinga na katika Manispaa ya Songea
nilizindua nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Shirila la
Nyumba la Taifa (NHC). Nyumba hizo za vyumba viwili na
vitatu zinauzwa kwa bei ya shilingi milioni 31 hadi 42.
Wenzetu wa NHC walinieleza utayari wa kujenga nyumba
zaidi endapo watapatiwa maeneo na Halmashauri za Wilaya na
Miji. Walinilalamikia kuwa hawapati ushirikiano wa kutosha
7
kutoka mamlaka husika. Nilipokuwa Mkinga na Songea
niliagiza Halmashauri hizo na nyinginezo nchini kutenga
maeneo kwa ajili ya NHC na Mifuko ya Hifadhi za Jamii yote ili
waweze kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wafanyakazi
na wananchi kwa ujumla.
Hii ni fursa ya aina yake kwa wananchi wa kipato cha
chini na cha kati kuweza kujipatia nyumba kwa urahisi.
Halmashauri zisiwe kikwazo wakati ardhi imejaa tele na kila
wakati wanapima viwanja vipya. Jambo lingine zuri
waliloniambia viongozi wa NHC ni kwamba zipo Benki
ambazo wanashirikiana nazo kutoa mikopo kwa watu
wanaonunua nyumba zao. Ni matarajio yangu kwamba
uongozi wa Halmashauri zote nchini utaitikia maelekezo
yangu na kwamba utatenga maeneo kwa ajili ya mashirika yetu
hayo.
Matibabu kwa Wazee
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa wilaya ya Kilindi nilifurahishwa sana na
utaratibu wa kuwapatia wazee huduma ya matibabu. Kama
8
mjuavyo Sera ya Afya inataka wazee na watoto wa chini ya
miaka mitano watibiwe bure katika hospitali za Serikali. Bahati
mbaya vitambulisho wanavyopata wazee vimekuwa
havithaminiwi ya kutosha. Kwa sababu hiyo, nafuu
wanayostahili kupata imekuwa haipatikani kwa urahisi na
wengine huikosa kabisa.
Katika Wilaya ya Kilindi, Halmashauri ya wilaya
imeamua kuwakatia wazee hao Bima ya Afya inayotolewa na
Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na hivyo kuondoa kabisa
migogoro inayohusiana na vitambulisho vya wazee
vilivyokuwepo kabla. Kwa kuzingatia malalamiko ya mara
kwa mara ninayoyapata kutoka kwa wazee kuhusu matibabu,
nashauri Halmashauri zote nchini ziige mfano wa Wilaya ya
Kilindi. Kama Kilindi wameweza kwa nini wengine
washindwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mikoa hii miwili nilipokea taarifa za kutia moyo
kuhusu juhudi za wananchi na Serikali katika kupanua fursa za
elimu. Vijana wengi wenye umri wa kujiunga na shule za
9
msingi wanafanya hivyo na wale wote wanaofaulu mtihani wa
darasa la saba wanapata fursa ya kwenda sekondari. Hatuna
tena tatizo la fursa. Pamoja na mafanikio hayo mazuri, taarifa
za wanafunzi wengi kushindwa kumaliza elimu ya msingi na
sekondari, zimenishtua na kunisikitisha sana.
Katika Mkoa wa Tanga kwa mfano, kati ya wanafunzi
50,921 walioanza darasa la kwanza mwaka 2007 , ni wanafunzi
41,017 tu ndiyo waliofanya mtihani mwaka 2013. Hivyo basi,
wanafunzi 9,904 ambao ni sawa na asilimia 19.4
hawakumaliza elimu ya msingi. Kwa upande wa sekondari,
katika mkoa wa Ruvuma, kwa mfano, kati ya wanafunzi 18,892
walioanza kidato cha kwanza mwaka 2010 ni wanafunzi 9,968
sawa na asilimia 52.76 ndiyo waliofanya mtihani wa kidato cha
nne. Hivyo basi, wanafunzi 8,924 sawa na asilimia 47.2
hawakumaliza elimu ya sekondari. Taarifa za namna hii
nilizipata pia katika ziara zangu ya Mikoa ya Kagera, Geita na
Simiyu. Nina kila sababu ya kuamini kuwa hali ni hiyo hiyo
kwa Mikoa mingine mingi nchini. Kwa kweli kiwango hiki cha
wanafunzi wanaoshindwa kumaliza elimu ya msingi na
10
sekondari ni kikubwa mno. Kinanisikitisha sana, hakikubaliki
na hakiwezi kuachwa kiendelee.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni yangu wazazi, walimu na viongozi wanao
wajibu maalumu wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote
wanahudhuria masomo shuleni tangu wanapoanza mpaka
wanapomaliza masomo yao. Huu ni wajibu wa lazima na siyo
hiari. Ni wajibu wa kisheria. Kwa hiyo, nimeagiza kwamba,
wazazi, walimu, Maafsa Elimu wa Wilaya wa Msingi na
Sekondari na Kamati husika katika Halmashauri zote nchini
ziwajibike ipasavyo kuhakikisha kuwa utoro mashuleni
unakomeshwa. Ajenda ya mahudhurio shuleni iwe ni ya
kudumu katika vikao vyote vya Halmashauri.
Kuanzia sasa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ni
lazima watoe taarifa za mahudhurio ya wanafunzi kwa Maafsa
Elimu wa Wilaya kila miezi mitatu. Maafsa Elimu wa Wilaya
nao watalazimika kutoa taarifa kwenye vikao vya Halmashauri
mwezi mmoja baada ya kupokea taarifa hizo. Halmashauri
hazina budi kuchukua hatua stahiki za kijamii na kisheria
11
kuhakikisha kuwa watoro wanarudi shuleni. Wazazi wa
watoto hao au mtu ye yote atakayebainika kuhusika na utoro
huo abanwe ipasavyo.
Sheria ya Elimu ya 1978 ipo, itumieni kwa ukamilifu
kulitatua tatizo hili. Haipendezi kusubiri mpaka miaka saba
kwa wanafunzi wa shule ya msingi au miaka minne kwa
wanafunzi wa sekondari ipite ndipo taarifa za utoro kwa
wanafunzi zitolewe au zijulikane. Lazima ufuatiliaji wa
mahudhurio uwe wa mara kwa mara ili hatua za kuzuia ziweze
kuchukuliwa mapema. Ninawataka viongozi wa TAMISEMI,
Mikoa na Wilaya kuchukua hatua stahiki kudhibiti tatizo hili la
utoro na watoto wengi kutokumaliza masomo. Litarudisha
nyuma maendeleo ya taifa.
Umeme Vijijini
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa mkoani Ruvuma nimezindua ujenzi wa
miradi mingi ya umeme vijijini. Kwa mujibu wa miradi hiyo
vijiji 309 vitapatiwa umeme kati ya vijiji 509 vya Mkoa huo
vinavyohitaji umeme. Napenda kutumia nafasi hii kutoa
12
pongezi za dhati kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof.
Sospiter Muhongo na viongozi wenzake, viongozi na
wafanyakazi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) pamoja na
TANESCO kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo ya kufkisha
umeme vijijini. Kwa kweli ni mara ya kwanza katika historia
ya nchi yetu suala la umeme vijijini kupewa msukumo mkubwa
kiasi hiki, kwani kinachofanyika Ruvuma kipo nchi nzima.
Nawaomba wananchi wanaofkishiwa umeme wautumie. Hata
gharama za kuunganisha umeme zimepunguzwa makusudi, ili
watu wengi waweze kumudu kuingiza umeme majumbani na
kwenye shughuli za kichumi na huduma.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama tujuavyo, Bunge Maalum la Katiba lililoahirishwa
tarehe 25 Aprili, 2014 kupisha Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi kushughulikia bajeti za
Serikali husika, litakutana tena tarehe 5 Agosti, 2014 kuendelea
na kazi yake ya kutunga Katiba Mpya. Kwa vile Bunge
Maalumu la Katiba halikuweza kumaliza kazi yake ndani ya
13
siku 70 zilizotengwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, nimeliongezea Bunge hilo siku 60 kwa ajili ya
kukamilisha kazi yake. Nimefanya hivyo kwa mujibu wa
mamlaka niliyopewa na Sheria hiyo hiyo.
Hatua Iliyofkiwa Kabla ya Kuahirishwa kwa Bunge
Ndugu Wananchi;
Itakumbukwa pia kuwa, tarehe 16 Aprili, 2014, baadhi ya
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hasa kutoka vyama vya
CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia mjadala
uliokuwa unaendelea Bungeni na kutoka nje. Wakati wanatoka
Bungeni, kazi kubwa ilikuwa imefanyika. Tayari Kamati zote
12 za Bunge hilo zilikuwa zimekamilisha kujadili Sura ya
Kwanza na ya Sita za Rasimu ya Tume. Sura hizo
zinazungumzia utambulisho wa nchi na muundo wa
muungano. Kamati zote zilipiga kura ya kupitisha uamuzi
wao kuhusu sura hizo mbili. Kamati kadhaa ziliweza kupata
theluthi mbili ya kura kwa Wajumbe wa pande zote mbili za
Muungano, jambo lililoonyesha dalili njema kwamba Katiba
mpya inaweza kupatikana.
14
Baada ya hapo, taarifa ya kila Kamati iliwasilishwa
kwenye Bunge zima. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge
Maalumu la Katiba, maoni ya wachache nayo yaliwasilishwa.
Kazi iliyokuwa inafuatia, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ni
kwa Kamati ya Uandishi kukamilisha taarifa yake na
kuiwasilisha kwenye Bunge zima kwa ajili ya kujadiliwa.
Baada ya Wajumbe kujadili taarifa hiyo itafuatia kupiga kura ili
kuamua kuhusu Sura hizo mbili. Kama yalivyo masharti ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uamuzi utafanywa kwa
theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano wetu.
Sababu za Baadhi ya Wajumbe Kususia
Bunge Maalumu la Katiba
Ndugu Wananchi;
Sote tumewasikia Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
waliosusia vikao vya Bunge hilo wakielezea sababu
zilizowafanya watoke Bungeni. Walitoa matamko kwenye
vyombo vya habari na pia katika mikutano ya hadhara
waliyoiitisha na kuhutubia sehemu mbalimbali nchini. Sababu
15
walizotoa zimekuwa zikiongezeka na kubadilika kadri siku
zinavyosonga mbele na upepo wa kisiasa unavyokwenda.
Hivi sasa wanazungumzia mambo mawili. Kwanza,
kwamba Bunge Maalumu halina mamlaka ya kuifanyia
mabadiliko yo yote Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa maoni yao, kazi ya Bunge
Maalumu la Katiba ni kujadili na kupitisha tu Rasimu ya
Katiba ya Tume na siyo kubadili cho chote. Pili, wametoa sharti
la wao kurudi Bungeni ni kuhakikishiwa kwamba,
kitakachojadiliwa Bungeni ni Rasimu ya Tume. Bila ya sharti
hilo kukubaliwa, wamesisitiza kutorudi Bungeni.
Mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba
Ndugu Wananchi;
Mimi nimehusika katika kubuni wazo la kuwa na
mchakato wa kuandika Katiba Mpya, na katika maandalizi ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ya kuongoza na kuendesha
mchakato huo. Kwa kweli sikumbuki wakati wo wote katika
vikao vya Baraza la Mawaziri kujadili Rasimu ya Muswada wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulipozungumzia Rasimu ya
16
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa haiwezi kufanyiwa
marekebisho na Bunge Maalumu la Katiba.
Mimi siyo Mwanasheria na hivyo nakiri kwamba naweza
kuwa na upungufu katika kuelewa maana ya baadhi ya
maneno ya kisheria. Hata hivyo, sikumbuki kuwepo kwa
kifungu cho chote katika Sheria kinachosema kuwa Bunge
Maalumu la Katiba halina mamlaka hayo. Tangu tulipoyasikia
maneno hayo yakisemwa nimeuliza nithibitishiwe ukweli wa
madai hayo bado sijaambiwa vinginevyo. Kama ukweli huo
upo naomba anisaidie. Badala yake naambiwa kuwa maneno
yaliyotumika katika Sheria haiakisi dhana inayotolewa kuwa
kazi ya Bunge Maalum la Katiba ni kubariki Rasimu na siyo
kufanya vinginevyo. Nimeambiwa kuwa sheria inasemaTume
itaanda Rasimu ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba
litatunga Katiba iliyopendekezwa.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 30 Desemba, 2010, nilipozungumzia dhamira
yangu ya kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya
nilieleza wazi nia ya kuwepo kwa uwakilishi mpana wa
17
Watanzania katika mchakato huo. Ndiyo maana katika Sheria
tukaweka ngazi nne katika mchakato wa kutunga Katiba.
Ngazi ya kwanza ikiwa ya wananchi kutoa maoni yao juu ya
kila wanachotaka kijumuishwe katika Katiba ya nchi yao.
Ngazi ya pili, ni ya wananchi kupitia wawakilishi wao katika
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na Mabaraza ya Kitaasisi kutoa
maoni yao kuhusu Rasimu ya kwanza ya Katiba
iliyotayarishwa na Tume.
Ngazi ya tatu inajumuisha wawakilishi wa wananchi
waliopo kwenye Mabaraza ya Kutunga Sheria ya Sehemu zetu
mbili za Muungano, yaani Bunge la Jamhuri ya Muungano na
Baraza la Wawakilishi, wakichanganyika na Wawakilishi wa
makundi mbalimbali ya jamii ya Watanzania kutoka pande
zote mbili za Muungano. Hawa ndio wanaounda Bunge
Maalumu la Katiba, lenye jukumu la kutunga Katiba
inayopendekezwa.
Mamlaka ya kutunga Katiba kwa mila na desturi za
Mabaraza ya Kutunga Sheria ni uwezo wa kurekebisha,
kubadili, kufuta na hata kuongeza kilichopendekezwa.
18
Ingekuwa kilichokusudiwa ni kubariki tu lisingetumiwa neno
la kutunga Katiba. Hali kadhalika, lisingewepo sharti la kupiga
kura na msisitizo wa kupata theluthi mbili kwa kila upande wa
Muungano. Aidha, kama ingekuwa jukumu la Bunge
Maalumu ni kubariki tu Rasimu lisingepewa siku 70 za kazi na
Rais kupewa mamlaka ya kuongeza siku zaidi kadri aonavyo
yeye inafaa.
Ngazi ya nne na ya mwisho, tuliweka kura ya maoni ya
wananchi kukubali au kukataa Katiba inayopendekezwa na
Bunge Maalumu la Katiba. Kama ingekuwa Rasimu ya Tume
haiwezi kubadilishwa hata nukta kwa nini basi tuweke kura ya
maoni ya kuwahusisha wananchi wote?
Ndugu Wananchi;
Tulizibuni ngazi hizi nne kwa dhana kwamba kile
ambacho hakikuonekana au hakikuwekwa sawa katika ngazi
moja kitaonekana na kurekebishwa katika ngazi inayofuata
katika ngazi zile tatu za mwanzo. Na, iwapo Katiba
iliyotungwa haitawaridhisha wananchi wanayo haki ya
19
kuikataa. Kwa kufanya hivyo, wananchi ndiyo waliopewa
turufu ya mwisho.
Ndugu wananchi;
Kwa kweli, napata shida kuelewa mkanganyiko unatoka
wapi na hasa wale wanaoongoza kuhoji mamlaka ya Bunge
Maalumu kuwa ni wale wale waliotunga Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba tena hatua kwa hatua. Nashangazwa zaidi ninapoona
wale wale waliotunga Kanuni za Bunge Maalumu ndiyo
wanaoongoza kuhoji uhalali wa kile walichokitunga.
Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, Ibara ya 33 (8)
inasema: Nanukuu: Wakati wa mjadala, Mjumbe yoyote
anaweza kutoa mapendekezo ya marekebisho, maboresho au
mabadiliko yaliyomo katika Sura za Rasimu ya Katiba
zinazojadiliwa kwa utaratibu ufuatao: (a) Ikiwa ni
marekebisho, maboresho au mabadiliko yanayobadilisha
jambo la msingi, au yanayobadilisha maudhui ya Ibara,
mapendekezo ya marekebisho yatapelekwa kwa maandishi
kwa Katibu siku moja kabla ya mjadala wa Ibara husika. (b)
Ikiwa ni marekebisho madogo, ambayo hayabadili msingi au
20
maana, mapendekezo ya marekebisho yatawasilishwa na
mjumbe wakati wa mjadala baada ya kupata ruhusa ya
Mwenyekiti. Mwisho wa kunukuu.
Kanuni hii ilipotungwa, Wajumbe wote wa Bunge
Maalumu pamoja na wale ambao baadae walisusia vikao vya
Bunge walikuwepo Bungeni na walishiriki kuipitisha. Tena
basi, baadhi yao walikuwa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni
iliyopendekeza Kanuni hizo. Unapowaona watu wale wale
sasa wanakuwa vinara wa kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu
la Katiba, unajiuliza maswali mengi kuhusu watu hao bila ya
kupata majibu yaliyo sahihi na kutosheleza akili na ufahamu
wetu.
Ndugu Wananchi;
Unaposoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za
Bunge Maalumu, hii ni dhahiri kwamba wote walikuwa na
uelewa wa pamoja kuhusu mamlaka ya Bunge Maalumu ya
kujadili Rasimu iliyoandaliwa na Tume na kutunga Katiba
inayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.
21
Kinachojadiliwa Bungeni ni Rasimu ya Tume
Ndugu Wananchi;
Yapo madai yanayotolewa na kuenezwa na Wajumbe
waliosusia Bunge Maalumu la Katiba kwamba kinachojadiliwa
Bungeni siyo Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ndiyo
maana basi wanaweka sharti la kujadiliwa Rasimu ya Tume ya
Jaji Warioba ndipo warudi Bungeni. Madai haya nayo yananipa
taabu kuyaelewa. Ndugu zetu hawa walishiriki siku zote 19 za
Kamati 12 zilipokutana kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita za
Rasimu ya Tume. Halikadhalika. walikuwepo na kushiriki kwa
ukamilifu wakati taarifa za Kamati, tangu ya Kwanza mpaka
ya 12, zilipowasilishwa kwenye Bunge zima. Aidha, na wao
walishiriki kutoa maoni ya wachache kwa dakika 20 na kutoa
ufafanuzi kwa muda wa dakika 30 kwa kila Kamati. Haya
maneno ya sasa kwamba kinachojadiliwa Bungeni siyo Rasimu
ya Tume ya Jaji Warioba bali nyingine kabisa ambayo wanadai
eti ni ya CCM yanatoka wapi.
Mimi nadhani kuwa huenda katika Kamati kumefanyika
marekebisho kwenye Rasimu ambayo hayakuwapendeza.
22
Kama hivyo ndivyo, wawe wakweli kuhusu jambo hilo kuliko
kusema mambo yasiyowakilisha ukweli halisi wa Rasimu
inayojadiliwa. Matokeo yake ni kuwafanya wafuasi wao na
wapenzi wao na hata watu wengine waamini kuwa
kinachojadiliwa siyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba bali
nyingine tena ni ya CCM. Jambo hilo si kweli na wenyewe
wanajua kwamba si kweli ila sijui kwa nini wameamua
kupotosha ukweli.
Ndugu Wananchi;
Kinachonishangaza, zaidi ni kwamba, kama
hawakuridhishwa na yaliyofanyika, kwa nini wasingetumia
mifumo waliyojitengenezea wenyewe kwenye Kanuni kumaliza
tofauti zao? Kanuni zinaelekeza kuwa mambo wasiyoridhika
nayo yajadiliwe kwenye Kamati ya Mashauriano na
Maridhiano. Ukiacha mifumo ya maridhiano ndani ya Bunge
ukaenda nje kwa wananchi au vyombo vya habari na mitandao
si jawabu la tatizo.
Ndugu Wananchi;
23
Ndiyo maana nashawishika kuunga mkono wale wote
wanaowasihi Wajumbe wa CHADEMA, CUF na NCCR-
Mageuzi na wengine warejee Bungeni. Watumie mifumo
maalum ya Bunge iliyowekwa na Kanuni kutafuta maridhiano.
Hali kadhalika, wasichoke kuwa na mawasiliano na vyama
vingine vya siasa na hasa CCM kutafuta maelewano. Mimi
niko tayari kusaidia pale watakapoona inafaa kufanya hivyo
kama ambavyo nimekuwa nikifanya ziku za nyuma.
Nililolisema mwanzoni kabisa mwa mchakato na
nalirudia tena leo kwamba, ili tuweze kufanikiwa kupata
Katiba Mpya ambayo sote tunaitaka, maelewano baina ya
wadau wakuu wa kisiasa ni jambo lisilokuwa na badala yake.
Vinginevyo kupata theluthi mbili kwa pande zote mbili za
Muungano haitawezekana. Ndiyo maana nampongeza sana
Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi,
kwa uamuzi wa kuvikutanisha vyama vinne vikuu vya siasa
kujadili namna ya kuondoa mtihani uliopo sasa katika
mchakato wa Katiba.
24
Ombi langu kwa viongozi wa vyama hivyo ni kuitumia
vyema fursa ya majadiliano kuukwamua mchakato kwa
maslahi ya nchi yetu na watu wake. Hali kadhalika
nampongeza sana Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Mheshimiwa Samwel Sitta, kwa kuitisha kikao cha Kamati ya
Mashauriano na Maridhiano. Bahati mbaya ni kwamba
Wajumbe wa vyama vilivyosusia Bunge Maalumu
hawakushiriki. Ni matumaini yangu kuwa Mheshimiwa Sitta
hatokata tamaa kuendeleza juhudi za mashauriano na kwamba
katika vikao vijavyo na wenzetu hawa watashiriki.
Ndugu Wananchi;
Hivi karibuni kumekuwepo pia madai yanayoelekeza
lawama kwangu. Kwanza nalaumiwa eti kuwa mambo
25
yalikuwa yanaenda vizuri mpaka pale nilipotoa hotuba ya
ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika. Pili
nalaumiwa kwamba nawezaje kuikana Rasimu ya Katiba
ambayo na mimi ni mmoja wa watu waliotia sahihi katika
Rasimu hiyo.
Niruhusuni nianze na hili la pili. Nadhani ndugu
zetu wanaotoa madai haya yameitafsiri isivyo sahihi yangu
katika Gazeti la Serikali lililotangaza rasmi Rasimu ya
26
Katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa
mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Tume
kumaliza kazi yake ya kuandika Rasimu ya Katiba, Rais
wa Jamhuri ya Muungano amepewa kazi tatu kufanya.
Kwanza, kupokea Rasimu hiyo na Taarifa ya Tume kutoka
kwa Mwenyekiti jambo ambalo lilifanywa tarehe 30
Desemba, 2013. Pili, amepewa kazi ya kuitangaza rasmi
Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume kwa watu wote
27
kuiona na kuisoma ndani ya siku 30. Alipewa sharti la
kuitangaza katika Gazeti la Serikali na vyombo vingine
vya habari. Hili nalo lilifanywa hivyo tarehe 22 Januari,
2014.
Ndugu Wananchi;
Katika kutangaza katika Gazeti la Serikali sharti
linamtaka anayetangaza ajitambulishe kuwa yeye ni nani
na atie sahihi yake. Kwa kufanya hivyo, hakumfanyi yeye
28
kuwa naye ni mhusika na maudhui ya kila
kinachopendekezwa na Tume. Sahihi zilizomo ndani ya
Rasimu na Taarifa ya Tume ni za Wajumbe wa Tume,
kamwe sahihi ya Rais haimo hivyo hawezi kulaumiwa
kuwa anaikana sahihi yake. Yeye ametimiza wajibu wake
wa kutangaza, akaiweka hadharini kwa umma wa
Watanzania kuiona na kusoma Rasimu ya Katiba na
Taarifa ya Tume vilivyotayarishwa na kutiwa sahihi na
29
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi ya tatu
ni kuitisha Bunge Maalumu ambayo nayo imekamilika
tangu tarehe 18 Februari, 2014.
Ndugu Wananchi,
Jambo lingine linalofanana na hilo ni yale madai
kwamba nilikuwa napata taarifa ya maendeleo ya
mchakato ndani ya Tume mara kwa mara, iweje leo nitoe
maoni tofauti kama niliyoyatoa katika hotuba yangu
30
kwenye Bunge Maalumu. Ni kweli kabisa Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph
Warioba, Makamu wake, Mheshimiwa Jaji Agustino
Ramadhani na Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed Salim
wamekutana na mimi kwa nyakati mbalimbali
kuzungumzia mwenendo wa mchakato. Lakini, hayakuwa
mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika
maudhui na mapendekezo ya Tume. Ukweli ni kwamba
31
Rasimu zote mbili nilizipata mara ya kwanza
nilipokabidhiwa rasmi, tena kwa uwazi. Napenda watu
wasijenge dhana kuwa nilipewa Rasimu na kuisoma kabla
ya kukamilika na hivyo nilitoa maoni yangu. Tume hii
ilikuwa huru na niliiacha iwe hivyo. Sikuiingilia kwa
namna yo yote ile kupenyeza mambo ninayotaka yawemo.
Kuthibitisha dhamira yangu ya kutaka Tume iwe huru
katika kufanya kazi zao hata pale waliponitaka nitoe
32
maoni niliwaomba tusifanye hivyo ili nisiwakwaze katika
kufanya kazi zao, wakapata taabu ya kuwianisha
wanayofkiria na mawazo yangu.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu madai kwamba mambo yalikuwa
yanakwenda vizuri na kwamba hotuba yangu iliyavuruga,
napenda kusema wazi kuwa lawama hizo hazina ukweli
wo wote. Ni madai yasiyokuwa na msingi. Kwani mimi
33
hasa siku ile nilifanya lipi la ajabu. Ukweli ni kwamba
nilisema yale yale ambayo Tume yenyewe imeyasema
katika Rasimu ya Katiba na Taarifa za Tume. Niliyoyasema
kuhusu malalamiko ya watu wa pande zetu za Muungano
na uzuri na changamoto za miundo ya Serikali mbili na
Serikali tatu ni yale yale yaliyomo kwenye taarifa za Tume.
Nimetumia takwimu zile zile za Tume. Pengine
34
kilichoonekana kuwa kibaya ni jinsi nilivyozifasiri taarifa
hizo na mapendekezo ya Tume.
Jambo lingine ambalo nimelifanya ni kutoa maoni
yangu kuhusu baadhi ya vipengele vya Rasimu hususan
uandishi na dhana mbalimbali zilizokuwamo. Silioni kosa
langu kwa kufanya hivyo, kwani Rasimu imetolewa
hadharani kwa watu kuijadili. Na mimi kama raia ninayo
35
haki ya kufanya hivyo kama wafanyavyo wengine. Kwa
nini nilaumiwe kwa kutumia haki yangu hiyo.
Lakini, pia mimi ndiye Rais wa nchi yetu, ninayo
dhamana ya uongozi na ulezi wa taifa letu. Itakuwaje kwa
jambo kubwa la hatma ya nchi yetu nilinyamazie kimya.
Watanzania wangeshangaa na wangekuwa na haki ya
kuhoji Rais wao ana maoni gani. Bahati nzuri nilitoa
maoni yangu mahali penyewe hasa, na kwa uwazi, kwenye
36
Bunge Maalumu la Katiba. Hata hivyo, ni muhimu
kusisitiza kuwa namna nilvyotoa maoni yangu sikuwa
natoa maagizo wala kushurutisha, ndiyo maana kila
wakati niliwakumbusha Wajumbe kuwa mamlaka ya
uamuzi ni yao. Yangu yalikuwa maoni tu wanahiyari ya
kuyakubali au kuyakataa. Niliwataka Wajumbe wasome
na kuielewa vyema Rasimu. Nilisema wasome sura kwa
sura, mstari kwa mstari na neno kwa neno. Niliwaomba
37
wajiridhishe kuhusu uandishi na dhana mbalimbali.
Nilitoa mifano ya mambo yahusuyo uandishi ambayo ni
vyema wayatazame. Pia nilitoa mifano ya dhana ambazo
niliwasihi wajiridhishe juu ya kufaa kwake kuwepo.
Kuhusu muundo wa Serikali tatu, nilieleza wazi
kuwa sina tatizo nao kama ndiyo matakwa ya Watanzania.
Lakini, nilieleza hofu yangu kuhusu mapendekezo ya
Tume na kuwataka Wajumbe wafanye kazi ya ziada
38
kuondosha udhaifu iwapo wataukubali muundo
unaopendekezwa. Nilieleza nia yangu ya kutaka tuwe na
Serikali ya Muungano yenye ukuu unaoonekana, yenye
nguvu ya kuweza kusimama yenyewe, inayoweza kuwa
tegemeo kwa nchi Washirika, Serikali isiyokuwa tegemezi
wala egemezi kwa nchi washirika na ambayo inavyo
vyanzo vya uhakika vya mapato. Hivi kwa kutoa ushauri
39
huo kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba inageuka
kuwa nongwa. Kwa kweli sielewi lawama ni ya nini?.
Naamini sistahili lawama bali pongezi kwa kuwa
muwazi na kutoa ushauri wa msingi ambao utasaidia nchi
kupata Katiba nzuri inayojali maslahi ya watu wa nchi yetu
na ya nchi zetu mbili zilizoungana miaka 50 iliyopita.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
40
Mwisho, ni maoni yangu ya dhati kuwa mgogoro
uliopo sasa katika mchakato wa Katiba hauna sababu ya
kuendelea kuwepo. Naamini hayo yote ambayo Wajumbe
wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wanayalalamikia
yanaweza kushughulikiwa kwa ukamilifu katika mifumo
ya Bunge Maalumu la Katiba iliyotengenezwa na Wajumbe
wote na wao wakiwemo. Nawasihi waitumie. Hali
kadhalika, kwa kupitia mazungumzo wanayofanya na
41
wenzao wa Chama cha Mapinduzi wanaweza kutengeneza
nguvu ya pamoja kutatua changamoto za sasa na
zitakazojitokeza baadaye. Kilicho muhimu ni kwa pande
zote kuwa na dhamira ya dhati ya kutoka hapa tulipo sasa.
Kama utashi wa kisiasa upo kwa kila mmoja wetu, hilo ni
jambo linalowezekana kabisa. Narudia kuahidi utayari
wangu wa kusaidia kadri inavyowezekana tusonge mbele.
42
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

You might also like